Jifunze Kuvuna Maarifa Ya Watu Wengine Yakusaidie Mahali Unapokwama

Naomba nianze kwa kukuliza swali, ni jambo gani hujafanikiwa kulifanya kwa sababu ya kukosa utaalamu (maarifa)? Mfano linaweza kuwa ni biashara, kilimo, ufugaji, uendeshaji wa miradi, uongozi, uandishi, uwekezaji,au jambo jingine lolote.

Kama kuna jambo la namna hiyo hujapata ufumbuzi wake na unakiu ya kulipatia ufumbuzi, makala hii  inakuhusu wewe. Hakuna haja ya kubaki unahangaika au kukata tamaa kwa sababu hiyo. Kuna mambo makubwa mawili ambayo yana kuhakikishia kuwa jambo linalokusumbua kwa kukosa utaalamu utaweza kupata utaalamu wake haraka sana.

Jambo la kwanza; Unaishi Katikati Ya Watu Wenye Utalaamu Unaoutaka.

Haijalishi unaishi wapi, mjini au kijijini ninauhakika kabisa kuna watu wengi sana wanakuzunguka kila mahali wenye uzoefu na utaalamu wa kutosha kwenye kitu unachokitaka. Hata kama watu hao hawako karibu yako lakini kwenye dunia ya sasa hakuna umbali kati yao na wewe. Ukiamua kuwatumia kila kitu unachokitaka utakipata.

Jambo la pili:  Teknolojia Inakurahisishia Kupata Chochote Unachokitaka.

Kukua kwa matumizi ya mtandao wa intaneti na simu ni fursa nyingine kubwa kabisa ya kukupa utaalamu wowote unaoutaka tena kwa haraka zaidi. Unachotakiwa ni kujifunza mbinu chache tu za kuvuna teknolojia hizi.

Mwanamama mashuhuri Mary Kay Ash, aliwahi kusema  kuwa “Kama unafikiri kuwa unaweza, kweli utaweza lakini ukifikiri kuwa huwezi, uko sahihi”

Mary Kay Ash anataka tumwelewe kuwa kufanikiwa kwa jambo lolote ni lazima uwe tayari na uamini kuwa unaweza tu, hata kama mazingira uliyonayo hayaonyeshi kama utaweza, lakini unatakiwa uwe na imani na ufanye juhudi. Lazima utapata unachokitaka.

Nikichukulia kwa mfano mimi nilipokuwa naanza kutengenza tovuti, nilijiona kabisa sina utaalamu huo lakini nilikuwa na kiu ya kutaka kutengeneza tovuti, kwa sababu hiyo nilifanya kila bidii na hatimaye sasa naweza kutengeneza tovuti ya aina yoyote tena kwa haraka zaidi.

Kuna mtu mmoja anaitwa Clarence Darrow aliwahi kusema kuwa, namnukuu; “Nilipokuwa bado mvulana mdogo nilikuwa naambiwa kuwa kila mtu anaweza kuwa Raisi. Sasa naanza kuamini”

Ukweli ndo huo, kwamba mtu yeyote anaweza kufikia kila nafasi na hadhi anayotaka bila kujali amesomea nini katika maisha yake. Kinachotakiwa ili mtu afikie huko anakotaka ni lazima ajifunze kuvuna maarifa ya watu wengine.

Zifuatazo ni mbinu kadhaa unaweza kuzitumia kuvuna maarifa ya watu wengine ili ujinasue na jambo lolote linalokukwaza.

Mbinu ya kwanza: Zungumza Na Mtu Mwenye Utaalamu Unaoutaka.

Hii ni mbinu unayoweza kuitumia kupata maarifa ya kila aina unayoyataka kutoka kwa wataalamu wa jambo unalolitaka. Mwombe nafasi ya kukutana naye mtu unayetaka kupata ujuzi kutoka kwake. Robert kiyosaki anasema yeye alikuwa anaandaa chakula cha mchana au cha jioni halafu anamkaribisha mtu anayetaka kupata ujuzi kutoka kwake, mara nyingi, mtu unapomwamdalia mazingira mazuri ya kuzungumza naye anajisikia vizuri na anaona unamthamini, uwe na uhakika atakushauri vizuri sana.  Kama yuko mbali mwombe “appointment” kwa njia ya email au hata kwa simu au kwa namna yoyote unayoweza kufanya.

Mbinu ya pili: Soma Vitabu, Sikiliza Rekodi Za Watu Mbalimbali Wanaoelezea Utalaamu Unaoutaka.

Kuna vitabu mamia kwa mamia duniani vinavyoelezea kila jambo unalotaka. Maarifa mengi sana yako vitabuni na kwenye rekodi za watu mabalimbali mfano filamu. Mbinu hii ya pili mimi binafsi imenisaidia sana, kila kitu ninachokitaka nakipata kwenye vitabu. Gundua njia yako ya maisha kwa kuvuna maarifa ya watu wengine. Kuna msemo usemao “the rich do invent their own way”

Mbinu ya tatu: Hudhuria Kwenye Semina, Warsha, Maonyesho Na Mikutano Mbalimbali Inayoelezea Kile Unachokitaka.

Nakumbuka tena maneno ya Robert kiyosaki kwenye kitabu chake “Retire Young Retire Rich” anasema ukitaka kutajirika mapema usiende shule nenda kwenye semina. Hapa, hana maana kuwa shule si kitu, hapana ila anasisitiza kwamba semina ni njia rahisi ya kujifunza mambo mengi na kwa haraka zaidi. Tena kwenye semina unajifunza kile tu unachotaka, shuleni unajifunza mambo mengi hata usiyoyataka.

Mbinu ya nne: Tembelea Sehemu Kilipo Kitu Unachotaka Kukifanya. Mfano kama unataka kujifunza kilimo cha uyoga kama unanafasi ya kutembelea mahali wanapolima uyoga nenda sehemu wanapolima uyoga, kwa macho yako utajifunza mambo yote.

Ikiwa kweli unataka kufanikiwa kimaisha uwezo huo unao wala huhitaji kuhangaika tumia maarifa ya watu wengine kufanikiwa. Kuna mamia ya njia halali za kufanikiwa, kama hutafanikiwa ni kwa sababu hujaamua tu. Chukua hatua sasa juu ya maisha yako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *